Tana Delta Inaorodheshwa Sehemu Ya Sita Chini ya Mapatano ya Ramsar

tana-map

Afisi ya Makubaliano ya Ramsar kuhusu Maeneo Lowevu imetangaza katika tuvuti yake kuorodheshwa kwa eneo la Tana Delta kama Eneo Muhimu Lowevu la Kimataifa tarehe 12 Oktoba 2012. Sehemu ya Tana Delta ina ukubwa wa hekta 163,600 lipatikanalo 02°27’S 040°17’E. Eneao hili linajulikana kama sehemu muhimu ya ndege katika Pwani ya Kenya na sehemu ya pili muhimu ya ki-ikolojia ya mdomo wa mto katika Africa Mashariki. Eneo hili lina sehemu tofauti tofauti ya mafuriko, mdomo wa mto, mazingira ya pwani yenye mikoko mingi, sehemu ya mchanganyiko wa maji ya bahari na majisafi, pwani safi na maeneo ya chini ya pwani ambayo kwa pamoja yanafanya mazingira mazuri zalishi.

Mazingira anuai ya Tana Delta inatoa nafasi kwa haidrolojia kukuza kamba, uduvi, samaki na aina tano za kasa walio katika hatari ya kuangamia, ndovu wa Africa na mbega wa eneo la Tana. Kuna aina zaidi ya 600 ya miti ambayo imetambuliwa ikiwemo Cynometra lukei na Gonatopus marattioides, aina mbili za miti ambayo iko katika hatari ya kuangamia. Tana Delta pia ni kituo muhimu cha malisho na majira ya baridi katika sehemu ya Asia Magharibi-Afrika Mashariki kwa ndege wa maeneo lowevu wanaohama hama.

Kwa sasa, Kenya ina maeneo sita muhimu yaliyo orodheshwa katika Mkataba wa Ramsar. Mbali na Tana Delta, maeneo yale mengine ni: –

1.Ziwa Nakuru
Ziwa Nakuru, moja ya maziwa yapatikanayo katika Bonde la Ufa, ni la kwanza kuorodheshwa kama eneo muhimu la Ramsar tarehe 5 Juni 1990. Lina ukubwa wa hekta 18,800 na linapatikana katika nyuzi 00º24’S 036º05’E. Eneo hili pia limeorodheshwa kama Turathi ya Dunia na Mbuga ya Kitaifa ya Wanyama Pori.

Ziwa Nakuru lina kina kidogo na lenye alikali kali. Ziwa lenyewe limezungukwa na pori na ukanda wa mbuga. Kuna mito minne ya msimu na mto wa kudumu wa Ngosur hujaza Ziwa Nakuru. Mazingira ya kinamasi, maeneo ya mafuriko na mwitu, imeweza kuhifadhi na kukuza aina nyingi za wanyama walio katika hatari ya kuangamia kama vile kifaru mweusi, kiboko na ndege aina ya African Darter (Anhinga rufa), Great Egret, Grey-crested Helmet-shrike, Lesser kestrel na Madagascar heron.

2.Ziwa Naivasha
Ziwa Naivasha liliorodheshwa kama Eneo Lowevu Muhimu la Ramsar tarehe 10 Aprili 1995. Lina ukubwa wa hekta 30,000 na lapatikana 00º46’S 036º22’E. Ziwa liko katika eneo la mwinuko katika Bonde la Ufa na ni moja ya maziwa yenye majisafi katika Afrika Mashariki. Eneo hili lina ziwa la shimo la volcano, delta ya mdomo wa mto na ziwa la kando la Oloiden lililojaa mchipwi wa kijani kibichi na miti inayostahimili magadi. Miti ya nchi kavu na ya maeneo lowevu inayopatikana katika eneo hili ni sehemu bora ya malisho na mazalio kwa aina zaidi ya 350 ya ndege wa maeneo lowevu wanaoishi hapa na wale wakuhamahama. Viboko, nyati na wanyama wengine wakubwa wa jamii ya mamalia wanapatikana hapa.

3.Ziwa Bogoria
Ziwa Bogoria ni la tatu kuorodheshwa katika Mkataba wa Ramsar nchini Kenya mnamo tarehe 27 Agosti 2001. Eneo la ziwa pia limetambuliwa kama Turathi ya Dunia na Hifadhi ya Kitaifa ya Wanyama Pori. Eneo hili lina ukubwa wa hekta 10,700 linalopatikana 00°15’N 036°05’E, upande wa mashariki ya Bonde la Ufa.

Maji ya ziwa ni ya magadi na lenye chemichemi za maji moto. Mazingira haya yameweza kukuza korongo wadogo wapatao milioni 1.5 na aina ya ndege wa maeneo lowevu wapatao aina 300. Mbuga hii pia imekuwa hifadhi ya tandala wakubwa.

4.Ziwa Baringo
Ziwa Baringo ni la nne kuorodheshwa kama eneo la Ramsar tarehe 10 Januari 2002. Lina ukubwa wa hekta 31,469 linalopatikana 00°32’N 036°05’E. Eneo hili pia ni Hifadhi ya Kitaifa ya Wanyama Pori na maji yake yenye chumvi kidogo ni muhimu kwa wakaazi wa sehemu hii kame ya Bonde la Ufa. Kisiwa cha kati cha Ol Kokwe ni cha mabaki ya volcano. Eneo hili lipo katika mfumo wa Bonde la Ufa linalopata maji kutoka kwa vyanzo vilivyoko milima ya Mau na Tugen.

Ziwa Baringo ni makazi na hifadhi kwa zaidi ya aina 500 ya ndege. Baadhi ya ndege wa kuhamahama ni wa muhimu kwa wanamazingira kwa minajili ya uhifadhi. Zaidi ya ndege 20,000 muhimu wameweza kunakiliwa katika eneo hili. Ziwa pia lina aina saba muhimu wa samaki, akiwemo perege aina ya Oreochromis niloticus baringoensis, anayepatatikana tu hapa.

5.Ziwa Elmenteita
Ziwa Elementaita liliorodheshwa kama eneo la Ramsar tarehe 5 Septemba 2005 na kama Turathi ya Dunia mwaka 2011. Eneo hili lina ukubwa wa hekta 10,880 linalopatikana 00°46’S 036°23’E. Ziwa hili ni la kina cha chini na maji yenye alikali. Maji ya alikali kwenye ziwa hili imekuza mchipwi ya samawati-kijani kibichi, Spirulina platensis, ambayo ni chakula kwa baadhi ya ndege. Zaidi ya ndege 610,000 wakiwemo aina 450 (80 wa maeneo lowevu) za ndege wameweza kuhesabiwa katika eneo hili. Takriban asili mia 28.5 ya korongo wadogo wote duniani wana makazi hapa. Na wakati wa kiangazi visiwa vya lava nyeusi huwa sehemu muhimu za mazalio kwa mwari wakubwa weupe katika Bonde la Ufa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *