Ziara ya Mafundisho kwa Mitambo ya Umeme wa Nguvu za Maji ya Meru na Embu

kam-meru

kam-meruKenya, kama nchi nyingine zinazoendelea, iko katika njia panda katika kukimu mahitaji ya kawi kwa kuendeleza uchumi na maendeleo. Uhaba wa kawi umeongezaka maradufu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mabadiliko ya mara kwa mara ya bei za mafuta.

Kupatikana kwa mafuta eneo la Turkana na gesi kidogo sehemu ya pwani ya Kenya si habari za kuridhisha sana kwa vile mchakato wa utoaji wa mafuta na gesi huchukua muda kabla iweze kupatikana na kutumika kusaidia uchumi wa nchi. Kwa upande mwingine, Kenya ina rasili mali nyingi ambazo zinaweza kutumika kuzalisha kawi inayohitajika kukuza uchumi na maendeleo. Na kinachotia moyo ni kwamba uzalishaji wa kawi hii inatumia malighafi isiyoisha. Kawi itokanayo na upepo, jua, fueli hai na mitambo midogo ya kawi ya nguvu za maji bado hazijatafitiwa vilivyo ili kujua uwezo wake nchini.

Ni kwa sababu hii ndio Shirika la Watengenezaji Bidhaa Kenya (Kenya Association of Manufacturers) katika mpango wa Kufadhili Uzalishaji na Matumizi Bora ya Kawi Inayotumia Malighafi Isiyoisha, waliandaa ziara ya siku moja ya mafundisho kwa Mitambo ya Umeme wa Nguvu za Maji ya Meru na Embu Ijumaa tarehe 30 Novemba 2012. Lengo kuu la ziara hii ilikuwa kuwaonyesha wadau mbinu mbadala za uzalishaji wa kawi kutumia nguvu za maji.

Ziara hii ilijumuisha wadau kumi na nane kutoka sekta ya maji, wakiwemo wawakilishi kutoka Shirika la Africa Nature, makampuni yanayosimamia maji katika mabaraza ya miji ya Nyeri, Thika, Nzoia, Kakamega na sehemu ya bonde la Ziwa Victoria. Katika ziara hii, kilichowavutia sana wadau ilikuwa ni uwezekano wa kuiga teknolojia hii ili kupunguza ongezeko la gharama ya kawi katika shughuli zao.

Msafara huu uliongozwa na Bw. Jeff Murithi Murage kutoka Shirika la Watengenezaji Bidhaa Kenya, na wadau walianza kwa kutembelea Kiwanda cha Majani Chai cha Meru kilicho chini ya usimamizi wa Shirika la Ukuzaji Chai Kenya (Kenya Tea Development Agency). Kiwanda hiki kiko kilomita 229 kutoka Nairobi na kilomita 23 kutoka mji wa Meru. Kiwanda hiki kiko mita 2000 juu kutoka usawa wa bahari na inapatikana kandokando ya misitu ya Mlima Kenya na Ithangune.

Bw. Benjamin Okole, Meneja Msimamizi wa Eneo hili, aliwatembeza wadau katika sehemu ya mradi wa uzalishaji umeme wa nguvu za maji uliokamilika mwaka wa 2008. Mradi huu ulianzishwa ili kukimu mahitaji ya umeme ya kiwanda cha majani chai. Kiwanda hiki huhitaji kilowati 720 kwa shughuli zake. Mtambo wa kuzalisha maji kwa nguvu za umeme wa Meru una uwezo wa kuzalisha kilowati 900 za umeme siku nzima kwa mtiririko wa maji ya kasi cha mita 1.5 mchemraba kwa sekunde (1.5m3/sec). Mradi wote uligharimu milioni 180, kiasi kikubwa kikitumika kunua arthi kutoka kwa jamii ili kutengeneza mtaro wa maji.

Mtambo wa kutengeneza kawi ya nguvu za maji unatoa maji yake kutoka mito ya Thingitu na Marimba kupitia mtaro wa mita 730. Mito hii ina vyanzo vyake katika Mlima Kenya. Mtaro huu una kina cha mita 1 na upana wa mita 3, na una uwezo wa kuweka maji mita 680 mchemraba ikiwa umejaa.

Mradi huu uliweza kukumbwa na changamoto kadhaa, kubwa kati yao ikiwa ni uhaba wa maji kutokana na matumizi ya maji ya mito na jamii. Kuna baadhi ya miradi ya maji ya jamii isiyo halali inayochukuwa maji kwa wingi. Hii imelazimu mtambo kufanya kazi kwa vipindi. Na wakati wa kiangazi, mtambo hufanya kazi kwa asilimia 40 ya uwezo wake kutokana na mtiririko wa maji wa kasi cha kati ya mita 0.6 na mita 0.8 mchemraba kwa sekunde.

Mbali na changamoto ilizokumba mradi, mtambo una uwezo wa kuregesha gharama yake katika kipindi cha miaka 10, umeweza kupunguza pa kubwa gharama ya kawi ya Kiwanda cha Chai cha Meru na kutumia tu umeme wa kitaifa kwa haja za dharura. Na msimu wa mvua, mtambo unatoa kawi ya kutosheleza kiwanda na hata kusambaza umeme wa ziada kwa fito umeme wa kitaifa

Baada ya kutembelea Kiwanda cha Chai cha Meru, wadau walitembelea kiwanda cha Kampuni ya Maji na Maji Taka ya Embu kilichoko kilomita 5 kutoka mji wa Embu. Kiwanda hiki kilijengwa kwa ufadhili wa watu wa Japan kama zawadi ya urafiki na uhusiano mzuri. Kiwanda hiki cha kisasa kinaweza zalisha kawi ya nguvu za maji kiasi cha kilowati 75 pamoja na kusafisha maji. Mitaro miwili sambamba inayounganisha chanzo cha maji na mitambo ina urefu wa kilomita tano. Kwa kusambaza maji, mtambo unatumia nguvu za mvuto wa muinuko wa arthi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *