0
Your Cart
No products in the cart.

Mwana Jamii Asili Halisi!

Mahojiano na Bi Martha Ntoipo


Ofisi ya Katibu Mkuu iliweza kufanya mahojiano na Bi Martha Lekitony Ntoipo, katika kuathimisha Siku ya Kimataifa ya Jamii Asili, inayo adhimishwa tarehe 9 Agosti kila mwaka.

 

Bi. Martha Ntoipo ni Mmaasai kutoka Wilaya ya Longido, kaskazini mwa Tanzania. Jamii ya Maasai wametambulika kama jamii asili kwa kuweza kuhifadhi mila na tamaduni zao kwa vizazi vingi. Bi Martha alikuwa katika familia kubwa ya kitamaduni ambapo babake ana bibi sita na watoto 60 (na bado wanaongezeka). Alibahatika kwenda shule, bila idhini ya babake, na kuepuka ndoa ya mapema.

 

Punde tu baadaya ya kumaliza masomo ya upili, Bi. Martha aliamua kutafuta suluhu ya changamoto alizozikumba na ambazo ni kizuizi kwa maendeleo ya watoto wasichana na wanawake kutoka jamii ya wa-Maasai. Maswala ambayo aliangazia zaidi ni ukeketaji wa wasichana, ndoa za mapema, elimu ya afya ya uzazi na jinsia, haki za kibinadamu, na haki za wanawake kumiliki mali na kufanya maamuzi.

 

Mnamo 2010, Bi Martha alianzisha shirika la Pastoralists Information and Development Organization (PIDO). Shirika la PIDO lina endeleza miradi ya afya, kujenga uwezo wa wanawake na uhifadhi wa mazingira.

 

Ijapo Bi. Martha amekuwa mstari wa mbele kumaliza desturi ya kukeketa wasichana, kuhimiza wasichana wa-Maasai kwenda shule na kujenga uwezo wa wanawake kufanya maamuzi mashinani, kitaifa na ngazi za kimataifa, yeye bado anathamini tamaduni bora za jamii asili. Ameweza kupata fursa kadhaa kuangazia maswala ya wanawake, jamii asili na mabadiliko ya hali ya hewa mashinani na hata katika ngazi za kitaifa na kimataifa, ikiwemo kongamano zilizo andaliwa na Umoja wa Mataifa.

 

Kwa mtazamo wake, Bi Martha anaona kubadilishwa kwa maeneo ya jamii asili kuwa hifadhi za Wanyama pori na vizuizi vinavyowekwa vya kuingia hifadhi hizi kutafuta lishe kwa mifugo na miti dawa kama changamoto kubwa kwa jamii asili. Changamoto hizi zimeshuhudiwa eneo la Ngorongoro ambapo vijiji vya wa-Maasai vilibadilishwa kuwa hifadhi za Wanyama pori. Kwa sasa, vijiji 136 wameregeshewa maeneo yao baada ya Rais John Magufuli kuingilia swala hilo. Maombi yake kwa Rais Magufuli ni kuwa ardhi katika vijiji vya jamii asili Wilaya ya Ngorongoro na Longido ambavyo vimetengwa kuwa hifadhi ya wanyama pori itaregeshwa kwa jamii hizo. Ana wasiwasi pia kuwa kwenda shule kumeathiri uwezo wa kizazi cha sasa kijifunza lugha na tamaduni zao za asili.

 

Dondoo Kutoka Kwa Mahojiano:

 

Ofisi ya Katibu: Je, ni mambo gani unayo yaona muhimu katika kujenga uwezo wa wanawake katika ngazi ya familia, jamii, kitaifa na hata kimataifa?

 

Bi. Martha Ntoipo: Wanawake wanakuwa na uwezo pale ambapo wanaweza kufanya maamuzi muhimu kuhusu miili yao, watoto wao na afya yao katika ngazi zote. Jambo hili linaweza faulu pale wanawake watakapo kuwa na haki za kiuchumi na kukaa katika vikao vya maamuzi muhimu ya kisiasa.

 

Ofisi ya Katibu: Kwa maoni yako, ni nini kinahitajika kufanywa ili kuleta maendeleo kwa jamii asili na wanawake?

 

Bi. Martha Ntoipo: Elimu, ikiwemo elimu ya ngumbaru na ya vyuo vya kiufundi, misaada na mikopo rahisi ya kuanzisha na kuendeleza biashara, kuanzishwa kwa vituo vya redio mashinani na ukuzaji wa lugha za kitamaduni ni baadhi ya mambo yanayo saidia kuendeleza jamii asili. Na kuongezea, wanawake kutoka jamii asili wanahitaji kusaidiwa ili waweze kung’ang’ania viti vya kisiasa.

 

Ofisi ya Katibu: Ni mawaidha gani unaweza kuwapa wanawake wanaopanga kuwa mstari wa mbele kutetea haki za jamii asili na wanawake?

 

Bi. Martha Ntoipo: Ningependa wajue kuwa wana uwezo wa kuwa wanachotaka kuwa. Kinacho kosekana ni ujasiri wa kuchukua hatua kutimiza ndoto zao. Ni muhimu wachukue HATUA hiyo. Ni muhimu pia wakumbuke kuwa sisi ndio tunaweza kuleta mabadiliko tunayo yataka, kwa hivyo tujihusishe kuleta mabadiliko hayo. Haki huja Pamoja na majikumu. Natufanye majukumu yetu ili tuweze kudai haki zetu.

Maoni Yako

Barua pepe yako haitachapishwa,

Chapisho za Hivi Karibuni

swSwahili