Subtotal: $5.00
BUSTANI ZA MATUMBAWE - Mbinu Mpya ya Kuboresha Mazingira ya Bahari
Bw. Abdalla Omar Juma, (Muandishi wa Makala) ni Katibu wa Wasini Beach Management Unit, kikundi cha kijamii kilichoundwa kufuatia sheria ya Usimamizi na Uendelezaji Uvuvi Kenya.
Bahari na rasilimali zake daima hushangaza. Ina aminika kuwa hatujavumbua siri nyingi ambazo bahari imeficha ukilinganisha na kile tunajua kuhusu rasilimaki za nchi kavu. Lakini kuna jambo moja ambalo sote tunalifahamu vyema. Kwamba bin Adam wameendelea kuharibu bahari kwa kiasi kikubwa mno kwa uchafuzi, hasa uchafuzi wa plastiki na umwagikaji wa mafuta baharini.
Hata ingawa bahari zetu si safi, zimeenedelea kuzalisha bidhaa na huduma ambazo zimesaidia maisha katika dunia. Ukamilifu na uzalishaji wa bahari umepigwa jeki na uvumbuzi wa mbinu mpya ya kurudisha upya maeneo ya bahari ambayo yameharibika kupitia upanzi wa matumbawe.
Jamii ya kisiwa cha Wasini ni miongoni mwa jamii za kwanza Afrika kufanya majaribio na kufaulu kupanda matumbawe. Majaribio haya yalitumia ujuzi asili na wa kisayansi kupanda vipande vya matumbawe katika kitalu (nasari) kabla kuhamisha katika sehemu zilizoharibika za bahari. Jamii ilisaidiwa na shirika la Africa Nature Organization, Shirika la Utafiti wa Bahari na Uvuvi Kenya na Idara ya Uvuvi.
Ina julikana kuwa sehemu za matumbawe ni sehemu muhimu za makao kwa aina nyingi za viumbe hai baharini. Zinatambulika kwa kutoa manufaa mengi ya kiuchumi, ki-ekolojia, urembo na tamaduni. Sehemu hizi pia ni muhimu kama mazalio na maficho ya samaki na viumbe hai vya baharini.
Kutokana na uharibifu wamaeneo ya bahari na binAdam kupitia uchafuzi, uvuvi usio endelevu na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, matumbawe yana zidi kupotea. Hii ni kwa sababu, matumbawe haya wezi ongezeko la joto baharini, asidi baharini, mawimbi, miale mikali ya jua na mrundiko wa mchanga. Uharibifu huu unachoma, kuua, kupunguza uwezo wa kuzaa na hata kuhatarisha matumbawe na magonjwa.
Mchakato wa kutengeneza bustani ya matumbawe huanza kwa kukuza vipande vya matumbawe katika kitalu ili kuyakinga na athari zinazokumba matumbawe yakiwa madogo. Baada ya kukuzwa katika kitalu, matumbawe yaliyokomaa hupandwa katika sehemu zilizo chaguliwa kwa minajili ya kuziregesha upya. Kwa sasa, utengenezaji bustani za matumbawe unatumiwa kama chombo cha kuregesha matumbawe sehemu zilizoharibiwa.
Kuna hatua 10 zilizotumiwa na jamii ya Wasini kutengeneza bustani za matumbawe. Nazo ni: -
- Kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuregesha upya sehemu zilizoharibika za matumbawe,
- Kutambua sehemu zilizoharibika za matumbawe kupitia ushirikiano wa jamii na wataalam, na kutoa ramani, kuzitenga sehemu hizi na kuorodhesha kazi za kipaumbele,
- Kufanya utafiti wa msingi kwa maeneo yaliyo lengwa kwa kukusanya habari kama vile wingi wa samaki, aina za samaki, shughuli za uvuvi na utalii, na kadhalika,
- Kutambua aina za matumbawe na sehemu za kutoa mbegu za matumbawe,
- Mafundisho kwa jamii na wadau wengine kuhusu mchakato wa kutengeneza bustani za matumbawe,
- Baada ya mafundisho, sehemu za kuweka vitaru zilichaguliwa na kutengezwa kutumia matofali,
- Mbegu za matumbawe zilikusanywa na kupandwa katika vitalu,
- Kufuatizia ukuaji wa matumbawe katika kitalu na kuhakikisha usafi ili kuongeza ukuwaji haraka wa matumbawe,
- Matumbawe yaliyo komaa katika kitalu yapandwa katika sehemu zilizo tengwa kwa upanzi wa matumbawe,
- Kufuatizia mara kwa mara ukuaji wa matumbawe katika bustani.
Kwa sasa, kuna ongezeko la manufaa kutokana na wingi wa samaki na watalii wanaotembelea bustani za matumbawe. Watalii wanatoka taasisi za elimu, watafiti na vikundi vya kijamii wenye hamu ya kuanzisha bustani zao.
Kuna mpango wa kupanua bustani za matumbawe katika kisiwa cha Wasini na sehemu nyinginezo katika pwani ya Kenya.