0
Your Cart
No products in the cart.

MSITU WA MADUNGUNI - Msitu Asili Wa Pwani Ya Kenya Unaoangamia Polepole 

Waandishi wa Makala: Bw. Raphael Ngumbao, Mwenyekiti, Friends of Madunguni Forest, na mwanachama, Watu Mazingira Ulimwenguni. 


Msitu wa Madunguni ni msitu wa serikali wenye eneo la heka 951.85. Msitu huu ni moja wa misitu asili ya sehemu kame za pwani. Unapatikana kaskazini mashariki mwa msitu mashuhuri wa Arabuko Sokoke. Barabara ya Malindi-Sala Gate inagawanya misitu hii miwili.Msitu wa Madunguni, ni hifadhi ya wanyama na miti asili inayopatika tu katika eneo hili la Madunguni-Arabuko Sokoke. Ni masilikitiko kuwa msitu wa Madunguni umeendelea kuzorota kutokana na uvamizi wa maskwota, watengeza makaa, wavuna mbao na wanao tafuta kuni za kuuza.

Ina kadiriwa kuwa asili mia 75 ya msitu umepotea tangu miaka ya 1980 kwa sababu ya uvamizi huu. Madhara yake yamekuwa mmomonyoko wa udongo unao athiri mashamba na makazi sehemu za chini ya Madunguni. Mmomonyoko huu umeleta maporomoko makubwa sehemu kadhaa za msitu.

Msitu wa Madunguni ulipata jina lake kutoka kwa kijiji cha Madunguni, kinacho julikana kwa mashamba yaliyo na rotuba na sehemu muhimu ya kuzalisha chakula kwa Kaunti ya Kilifi. Dungu, ambapo wingi wake ni madungu, ni nyumba iliyo inuliwa kwa miti ili kukinga wakulima dhidi ya uvamizi wa simba na wanyama wengine wa pori.

Msitu wa Madunguni awali ulikuwa chini ya usimamizi wa Serikali za Wilaya. Na kwa wenyeji wa Madunguni waliuhifadhi kwa sababu ya kupata kuni kwa vile hawakuwa na ruhusa ya kuingia katika msitu wa Serikali wa Arabuko Sokoke. Lakini muhimu zaidi ni kwamba, wenyeji walitumia msitu huu kutabiri mvua na hali ya hewa. Na kwa hivyo, palikuwa sehemu takatifu kwa wenyeji.

Lakini mambo yalianza kubadilika kuanzia 1969. Wakaazi wa eneo la Maili 10 ya pwani, ikijulikana wakati huo kama Mikaoni, walianza kuvamia msitu wakitafuta kuni, mbao, kulima na hata kutengeneza makaaa. Sehemu ya Mikaoni ilijumuisha vijiji vya Kakuyuni, Mere na Mida.

Mnamo 1971, jamii ya Madunguni pamoja na Afisa wa Misitu, Bw. Tinga, waliarifu Serikali ya Mkoa kuhusu uharibifu huu. Machifu Awadh na Athmani Ndurya, wa sehemu ya Mikaoni, walipewa jukumu la kusitisha uharibifu huu kutoka kwa wakaazi wanaotoka sehemu zao. Kutokana na ushirikiano wa Afisa wa Misitu na jamii ya Madunguni, kijiji cha Madunguni waliweza kuunda Kamati ya Mazingira ya Madunguni.

Mwaka huu pia Idara ya Misitu ilinuia kujenga kituo kidogo cha utafiti eneo la Arabuko Sokoke ndani ya Msitu wa Madunguni. Lakini wenyeji wa Madunguni wakiongozwa na mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira ya Madunguni, Bw. Ngumbao Mwanzili, hawa kukubaliana na wazo hilo. Wangekubali, pengine msitu wa Madunguni ungebadilishwa kuwa wa Serikali.

Kufikia 1980, uharibifu wa msitu ulikuwa umekithiri. Bw. Ngumbao Mwanzili alipata kuungwa mkono na Bw. Kaingu Bindurya na Abdalla Ndema, wakereketwa waliosaidia kuhamasisha jamii kuhusu uharibifu wa msitu. Kwa juhudi zao, wavamizi walifurushwa na Serikali ya Mkoa na kujipatia makao karibu na msitu. Kufikia 1987, wavamizi walirudi tena kufanya makao na kuendelea kulima ndani ya msitu.

Idadi ya wavamizi iliendelea kuongezeka hadi 500 mwaka wa 1996. Wanasiasa pia wakaingilia swala la msitu wa Madunguni na kuwapa moyo wavamizi kuendelea kulima. Hali ilibadilika wakati wavamizi wa zamani na wapya walipoanza kuteta wenyewe kwa wenyewe. Wengine walipoteza maisha yao katika vita hivyo.

Serikali ya Mkoa ilishindwa kukabiliana na mwingilio wa wanasiasa katika kutatua mzozo wa msitu. Hatimaye, iliwabidi kuwafurusha wavamizi badala ya kuwapeleka kortini ambako wanasiasa walisaidia kurushwa kwa kesi zao.

Vijana wa Madunguni pia hawa kuachwa nyuma katika harakati za kuokoa msitu wao. Mnamo 2001, vijana waliunda na kusajili Friends of Madunguni Forest, kama njia moja ya kusaidia juhudi za Kamati ya Mazingira ya Madunguni. Mwaka 2004, pamoja na wadau wengine waliweza kumshawishi Mbunge wa Malindi, Bw. Abubakar Badawy kupeleka mswada bunge wa kubadilisha msitu huo kuwa wa Serikali. Na ombi hilo likapitishwa.

Wavamizi nao hawa kuachwa nyuma. Waliweza kupeleka kesi kortini kupinga kuorodheshwa kwa msitu kuwa wa Serikali. Korti iliamuru wavamizi wabaki bila kufanya shughuli zozote ndani ya msitu hadi kesi itakapo amuliwa.

Kesi bado haija amuliwa. Kwa muda huu, msitu umeendelea kuharibiwa bila kujali amri ya Korti.

Ukulima, utengenezaji makaa, na ujenzi wa shule, makanisa na msikiti zimeendelea ndani ya msitu. Idadi ya wavamizi pia imezidi kuongezeka hadi takriban watu 2000, na wana amini kuwa siku moja Serikali itachoka na kuwaachia msitu.

Kulingana na shughuli zote zinazo endelea ndani ya msitu, inakadiriwa kuwa msitu wa Madunguni utaangamia chini ya miaka 5. Athari kubwa Zaidi haitakuwa tu kwa msitu, bali pia kwa wakaazi wa Madunguni ambao mashamba yao yamepoteza rotuba kutokana na limbikizo la udongo usio rotuba kutoka msituni.

Maoni Yako

Barua pepe yako haitachapishwa,

Chapisho za Hivi Karibuni

swSwahili